Kifua kikuu (TB) ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na bakteria ajulikanae kama Mycobacterium tuberculosis. TB huathiri zaidi mapafu, lakini pia inaweza kuathiri sehemu nyingine za mwili kama mifupa, ubongo, figo na tezi.
Maambukizi ya TB husambazwa kupitia hewa, hasa mtu anapokohoa, kupiga chafya au hata kuongea akiwa na TB iliyo hai (active TB). Kwa kuwa TB ni hatari na inaweza kuambukiza watu wengi kwa haraka, ni muhimu kujua namna ya kujikinga nayo.
NJIA 10 ZA KUJIKINGA NA KIFUA KIKUU
1. Chanjo ya BCG kwa watoto wachanga
Chanjo ya BCG (Bacillus Calmette–Guérin) hutolewa kwa watoto wachanga mara baada ya kuzaliwa. Hii husaidia kupunguza hatari ya kupata TB sugu au kali hasa kwa watoto.
2. Epuka kuwa karibu na watu wenye TB ya mapafu
Ikiwa kuna mtu anaugua TB, jaribu kuweka umbali wa kutosha naye, hasa katika kipindi cha matibabu ya awali. Weka hewa safi na wazi mara kwa mara.
3. Funika mdomo na pua wakati wa kukohoa au kupiga chafya
Matone madogo yanayotoka mdomoni na puani ndiyo yanaweza kusambaza bakteria wa TB. Matumizi ya tishu au kitambaa huzuia kuenea kwa maambukizi.
4. Hakikisha hewa ya ndani inazunguka vizuri
Vyumba vya nyumbani, ofisini, au darasani viwe na madirisha na milango inayoruhusu hewa kuingia na kutoka. Bakteria wa TB huishi zaidi katika mazingira yasiyo na hewa ya kutosha.
5. Vaa barakoa katika maeneo ya hatari
Unapokuwa hospitalini, gerezani au mahali palipojaa watu na kuna uwezekano wa kuwa na mgonjwa wa TB, barakoa inaweza kusaidia kupunguza uwezekano wa kupata maambukizi.
6. Tumia dawa kwa usahihi kama umeambukizwa
Ikiwa umepatikana na TB, tumia dawa zako kikamilifu kama ulivyoelekezwa. Kutotumia dawa ipasavyo kunaweza kusababisha kuenea kwa TB sugu isiyotibika kirahisi (MDR-TB).
7. Fanya vipimo mapema endapo una dalili za TB
Dalili kama kikohozi cha zaidi ya wiki 2, homa ya usiku, jasho jingi, kupungua uzito na uchovu ni ishara za TB. Kufanya vipimo mapema husaidia kuanza matibabu mapema na kuepuka kuambukiza wengine.
8. Usikubali kuishi au kulala chumba kimoja na mgonjwa asiyeanza matibabu
TB huambukiza kwa haraka kama mgonjwa hajaanza dawa au anatumia dawa bila mpangilio sahihi. Hakikisha unachukua tahadhari hadi mgonjwa atakapothibitika kutokuwa na hatari.
9. Jenga kinga ya mwili kwa kula lishe bora
Lishe bora na yenye virutubisho vya kutosha husaidia mwili kupambana na maambukizi, ikiwemo TB. Kula mboga za majani, matunda, protini, nafaka na kunywa maji ya kutosha.
10. Punguza msongamano wa watu katika nyumba au maeneo ya kazi
Watu wengi wanaoishi au kufanya kazi katika mazingira yenye msongamano, kama vile magereza, migodi au hosteli, wapo katika hatari kubwa ya kuambukizwa. Fanya mpango wa kuishi katika mazingira yenye nafasi na hewa ya kutosha.
MASWALI YANAYOULIZWA MARA KWA MARA (FAQs)
Je, chanjo ya BCG inalinda watu wazima dhidi ya TB?
Chanjo ya BCG inalinda hasa watoto wachanga dhidi ya TB kali, lakini si madhubuti kwa watu wazima. Hata hivyo, ni hatua muhimu kwa watoto.
Ni lini mtu aliyepata TB si hatari tena kwa wengine?
Mgonjwa wa TB anakuwa si muambukizi tena baada ya kutumia dawa kwa wiki 2 hadi 3 kwa usahihi. Hii inaweza kutofautiana kwa kila mtu.
Je, TB huambukiza kwa kugusa?
Hapana. TB huambukizwa kupitia hewa, si kwa kugusa ngozi au kushikana mikono.
Je, barakoa za kawaida zinaweza kuzuia TB?
Barakoa za N95 ndizo bora zaidi kuzuia maambukizi ya TB, lakini hata barakoa za kawaida husaidia kupunguza hatari kwa kiasi fulani.
Je, TB inaweza kuzuiwa kwa kutumia dawa kabla ya kuugua?
Ndiyo. Watu waliokaribiana na mgonjwa wa TB, hasa watoto au watu wenye kinga hafifu, wanaweza kupewa dawa za kuzuia maambukizi (preventive therapy).