Mwongozo huu ni nyenzo muhimu ya kumsaidia mwombaji wa pasipoti au Hati ya
kusafiria kufahamu vigezo na hatua mbalimbali anazotakiwa kufuatwa ili kupata
huduma husika. Aidha, mwombaji ambaye anahitaji maelezo ya ziada au ufafanuzi
zaidi kuhusu huduma ya pasipoti na masuala mengine ya kiuhamiaji anaweza
kufika katika Ofisi yoyote ya Uhamiaji iliyo karibu naye.
AINA ZA PASIPOTI
Idara ya Uhamiaji inatoa aina mbalimbali za Pasipoti kwa raia wa Tanzania ambazo
ni; Pasipoti ya kawaida (Ordinary Passport), Pasipoti ya kiutumishi (Service Passport)
na Pasipoti ya Kidiplomasia (Diplomatic Passport)
PASIPOTI YA KAWAIDA (ORDINARY PASSPORT)
Pasipoti hii hutolewa kwa raia yeyote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
madhumuni ya kusafiri nje ya nchi. Pasipoti hiyo hutolewa, ikiwa na uhai wa muda
wa miaka kumi. Aidha, ikiisha muda wake wa matumizi au kujaa, mmiliki
anaruhusiwa kuomba pasipoti nyingine. Rangi ya pasipoti hii ni bluu (sky blue).
Pasipoti hii anaweza kuitumia kwenda nchi zote duniani.
PASIPOTI YA KIUTUMISHI (SERVICE PASPORT)
Pasipoti hii hutolewa kwa raia yeyote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
amabaye ni kiongozi katika Serikali ambaye ameainishwa kwenye Sheria ya Pasipoti
na Hati za Kusafiria, Sura ya 42. Pasipoti hiyo hutolewa ikiwa na uhai wa muda wa
miaka mitano na mwonekano wake ni rangi ya kijani. Pasipoti hii anaweza kuitumia
kwenda nchi zote duniani.
PASIPOTI YA KIDIPLOMASIA (DIPLOMATIC PASSPORT)
Pasipoti hii hutolewa kwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni
kiongozi katika Serikali mwenye hadhi maalum ya kupewa Pasipoti hiyo kama ilivyo
ainishwa kwenye sheria ya Pasipoti na Hati za Safari Sura 42. Pasipoti hiyo
hutolewa ikiwa na uhai wa muda wa miaka mitano na mwonekano wake ni raingi
nyekundu. Pasipoti hii anaweza kuitumia kwenda nchi zote duniani.
Mwombaji aliyepewa Pasipoti ya kiutumishi au kidiplomasia, endapo atastaafu au
kujiuzulu au kuondolewa kwenye nafasi iliyompa sifa ya kupatiwa pasipoti hiyo,
atapaswa kuirudisha kwenye mamlaka husika (Uhamiuaji) na endapo atahitaji
kusafiri nje ya nchi, atatumia pasipoti ya kawaida (Ordinary Pasipoti).
AINA ZA HATI ZA SAFARI
Idara ya Uhamiaji Tanzania inatoa aina tatu za hati za safari ambazo ni; Shahada
ya Dharura ya kusafiria, Hati ya Utambulisho (Certificate of Identity) na Hati ya
kusafiria ya Mkutano wa Geneva (Convention Travel Document)
HATI YA KUSAFIRIA YA DHARURA (EMERGENCY TRAVEL DOCUMENT)
Hati hii hutolewa kwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ana
safari ya dharura lakini hajakamilisha taratibu za kupata pasipoti ya kawaida. Aidha
hati hutolewa pia kwa raia wa Tanzania anayetaka kusafiri nje ya nchi na hawezi
kupata pasipoti kwa muda muafaka. Vilevile hati hii hutolewa kwa raia aliye kwama
nje ya nchi au anayerudishwa nchini kutoka nchi za nje.
Hati hii hutumika mara moja tu, yaani kwenda katika nchi husika na kurudi nchini.
Mara baada ya kurejea nchini, mmiliki ataikabidhi shahada hii kwa Afisa Uhamiaji
katika kituo husika cha kuingilia nchini.
Shahada hii ya dharura hutolewa katika Ofisi zote za Uhamiaji za mikoa na Ofisi
zote za Uhamiaji za Wilaya
HATI YA UTAMBULISHO (CERTIFICATE OF IDENTITY)
Hati hii hutolewa kwa mtu ambaye siyo raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
ambaye hawezi kupata pasipoti kutoka katika nchi ambayo ni raia au ambaye hana
uraia wa nchi yeyote kwa madhumuni ya kusafi nje ya Jamhuri ya Mungano wa
Tanzania. Hati hii hutolewa katika Ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu na Afisi Kuu
Zanzibar.
HATI YA KUSAFIRIA YA MKUTANO WA GENEVA (GENEVA
CONVENTION TRAVEL DOCUMENT).
Hati hii hutolewa kwa mkimbizi aliyepewa hifadhi ndani ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ambaye ana hitaji kusafiri nje ya nchi baada ya kukidhi vigezo kwa
mujibu wa Sheria Wakimbizi ya Mwaka 1998. Hati hii hutolewa katika Ofisi ya
Uhamiaji Makao Makuu na Afisi Kuu Zanzibar baada ya kupata uthibitisho kutoka
Idara ya wakimbizi.
ADA NA GHARAMA ZA HUDUMA ZA PASIPOTI
ADA YA HUDUMA ZA PASIPOTI
SN | AINA YA PASIPOTI/HATI | ADA | |
ILIYOOMBWA NCHINI | ILIYOOMBWA NJE YA NCHI | ||
1. | Pasipoti ya Kawaida | 150,000 Tsh | 90 USD |
3. | Pasipoti ya Kiutumishi | 150,000 Tsh | 90 USD |
4. | Pasipoti ya Kidiplomasi | 150,000 | 90 USD |
5. | Hati ya Dharura ya Safari | 20,000 Tsh | 20 USD |
Certificate of Identity | 10,000 | N/A | |
Hati ya Safari kwa Wakimbizi | 20,000 | N/A |
NB:
Kwa maelezo zaidi kuhusu aina za pasipoti, vigezo na namna ya kuomba tafadhali soma Mwongozo wa huduma za Pasipoti.
MAWASILIANO
Ukiwa na tatizo katika kuomba pasipoti au hati tafadhali wasiliana nasi kupitia baruapepe ifuatayo:
info@immigration.go.tz AU passporttanzania@immigration.go.tz
JINSI YA KUOMBA PASIPOTI
Mtu anayetaka kuomba Pasipoti ya Tanzania anatakiwa kutembelea tovuti ya Idara
ya Uhamiaji (www.immigration.go.tz), kisha anakwenda kwenye e-Services, ana
bofya Online Passport Application Au anaweza kuipata fomu hiyo moja kwa moja
kwa kubofya linki ifuatayo:
https://eservices.immigration.go.tz/online/passport
i. Baada ya kuingia kwenye ukurasa wa maombi ya pasipoti, mwombaji
ambaye ndio anaanza kujaza fomu yake atachagua OMBI JIPYA. Ikiwa
mwombaji alishaanza kujaza fomu akaishia katika hatua fulani, anapotaka
kuendelea atachagua ENDELEZA OMBI. Na ikiwa alishajaza na kukamilisha
fomu yake, na sasa anataka kuangalia maendeleo ya ombi lake atachagua
ANGALIA OMBI
ii. Kwa mwombaji anayeanza kujaza fomu yake, baada ya kuchagua OMBI
JIPYA, katika ukurasa utakaofunguka atahitajika kufanya uchaguzi wa Aina
ya Ombi. Ikiwa mwombaji hakuwahi kuwa na pasipoti atachagua OMBI
JIPYA. Ikiwa mwombaji aliwahi kuwa na pasipoti na sasa imejaa, au alikuwa
na pasipoti ya zamani sasa anahitaji pasipoti ya kielektroniki atachagua
PASIPOTI IMEJAA/IMEISHA MUDA WAKE/KUPATA PASIPOTI NYINGINE.
Ikiwa mwombaji alipoteza pasipoti yake ya awali atachagua PASIPOTI
ILIYOPOTEA na ikiwa pasipoti yake imeharibika au kuungua moto atachagua
PASIPOTI ILIYOHARIBIKA/KUUNGUA MOTO;
iii. Baada ya kuchagua aina ya ombi, mwombaji atajaza taarifa zake kwa usahihi
na ukamilifu;
iv. Kisha ataambatisha picha na viambato vinavyohitajika;
v. Baada ya kukamilika kwa hatua zote, mwombaji atapatiwa fursa ya kuhakiki
taarifa alizojaza na baada ya uhakiki atatakiwa kuthibitisha taarifa hizo kwa
kuweka alama ya vema (tick) kwenye chumba cha fomu kwenye mahali pa
Tamko “Declaration”;
vi. Baada ya kuthibitisha taarifa za mwombaji, atapatiwa Namba ya
kumbukumbu ya malipo (control number) ya Tsh 20,000. Kwa mwombaji
aliyeomba akiwa nje ya nchi atapatiwa ada yote kwa mkupuo ambayo ni USD
90;
vii. Baada ya kulipia, mwombaji atachapisha fomu yake na kuiwasilisha pamoja
na vielelezo vingine katika Ofisi ya Uhamiaji ya mkoa iliyo karibu naye au
ofisi ya Uhamiaji Kurasini au Afisi kuu Zanzibar;
viii. Mara baada ya Afisa kujiridhisha na vielelezo na maelezo ya mwombaji,
atampatia Namba ya kumbukumbu ya malipo (control number) ya Tsh
130,000;
ix. Baada ya mwombaji kulipia, ombi lake litapokelewa na atatakiwa Kwenda
kupiga picha na kuchukuliwa alama za vidole (fingerprints);
x. Baada ya kukamilisha hatua hiyo mwombaji atajulishwa siku ambayo
atatakiwa kufika Ofisini kuchukua pasipoti yake.
ZINGATIA
Mwombaji anatakiwa kuwa makini wakati wa kuchagua Aina ya Ombi kwa kuwa
viwango vya ada vinatofautiana kulingana na uchaguzi husika. Mwombaji yeyote
atakayefanya uchaguzi kimakosa, hatokuwa na nafasi ya kuja kudai ada ya mwanzo
ili kulipia uchaguzi tofauti. Badala yake atalazimika kujaza fomu nyingine kwa
usahihi
JINSI YA KUFANYA MALIPO
i. Malipo yote ya huduma hii yafanyike kupitia Namba ya kumbukumbu (Control
Number) iliyotolewa;
ii. Malipo yanaweza kufanyika kwa njia ya simu ya mkononi au kwa njia ya benki;
iii. Malipo yazingatie aina na kiasi cha fedha kilichoainishwa kwenye Namba ya
kumbukumbu ya malipo.
iv. Malipo ya huduma iliyoombwa nje ya nchi yafanyike kwa kutumia kadi
(Mastercard/Debit card) au kwa njia ya benki (Swift Transfer)
MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA WAKATI WA KUJAZA FOMU
i. Kabla ya kuanza kujaza fomu, hakikisha unavyo vielelezo vyote
vinavyohitajika.
ii. Taarifa za mwombaji zijazwe kwa herufi kubwa.
iii. Hakikisha taarifa za mwombaji wa pasipoti zinajazwa kwa usahihi na kwa
ukamilifu;
iv. Hakikisha majina yanayojazwa yanafanana na yale yaliyomo kwenye cheti
cha kuzaliwa au kiapo cha kuzaliwa mwombaji;
v. Ikiwa majina yanatofautiana kiapo cha kawaida au au kiapo cha kubadili
majina (Deedpoll) kitahitajika kutegemeana na utofauti wa majina uliopo.
vi. Endapo mwombaji atagundua tatizo lolote kwenye taarifa alizojaza baada ya
kuwa amekamilisha na kuchapa (print) fomu yake, atapaswa kurekebisha
taarifa husika kwa kutumia kalamu ya wino na kisha kusaini mbele ya taarifa
mpya iliyoingizwa;
vii. Mwombaji ambaye Pasipoti yake itabainika kuwa na makosa baada ya
kuchapwa, atawajibika kujaza fomu nyingine na kulipa ada kamili ya pasipoti
(Tsh. 150,000/-) ili aweze kupatiwa pasipoti nyingine;
viii. Malipo ya ada ya pasipoti yafanywe kwa kutumia namba husika ya
kumbukumbu ya malipo (Control Number) iliyotolewa baada ya kukamilisha
kujaza fomu;
ix. Baada ya fomu kukamilika na kuchapwa (printed) mwombaji atapaswa
kukamilisha taarifa katika kifungu cha 7 na cha 9. Kifungu cha 7 kitajazwa na
wadhamini wa mwombaji na kutiwa sahihi. Na kifungu cha 9 kitajazwa na
Hakimu, Jaji, Wakili au Kabidhi Wasii (mmojawapo) na kisha atagonga
muhuri.
x. Mwombaji ambaye atalazimika kutumia kiapo cha kuzaliwa badala ya cheti
cha kuzaliwa, ahakikishe kiapo husika kinaambatishwa na stempu ya ushuru
kama inavyoelekezwa na Sheria ya Viapo;
xi. Mwombaji ambaye ana umri chini ya miaka 18, wakati wa kuwasilisha fomu
yake Ofisini atapaswa kufika na mzazi au mlezi wake anayetambulika kisheria.
VIAMBATO VYA MWOMBAJI WA PASIPOTI
Mwombaji wa pasipoti anapaswa kuambatisha nyaraka za kuthibitisha uraia wake
na pia nyaraka za kuthibitisha shughuli anazofanya. Aidha, ikiwa mwombaji hana
shughuli yoyote anayofanya atalazimika kuthibitisha safari aliyonayo.
VIAMBATO VYA MSINGI
i. Cheti cha kuzaliwa mwombaji au cheti cha Tajnisi;
ii. Cheti au kiapo cha kuzaliwa mmoja wa mzazi wa mwombaji au cheti cha
Tajnisi;
iii. Kitambulisho cha Taifa (NIDA);
iv. Nakala ya pasipoti ya mzazi (kama anayo);
v. Barua ya maombi.
VIAMBATO VYA ZIADA VINAVYOWEZA KUHITAJIKA
i. Uthibitisho wa shughuli anazofanya mwombaji, mfano kitambulisho cha
kazi na barua ya mwajiri kumtambulisha mwombaji pasipoti, Leseni ya
udereva kwa wanaofanya kazi ya udereva, au leseni ya biashara au TIN
Number kwa wafanyabiashara n.k AU;
ii. Barua toka Serikali ya Mtaa inayothibiisha ukaazi wa mwombaji;
iii. Vielelezo vya elimu kwa mwombaji anayetaka kusafiri kwa ajili ya
masomo, AU
iv. Vielelezo vya ugonjwa kwa mwombaji anayetaka kusafiri kwa ajili ya
matibabu
v. Kwa mwombaji wa pasipoti ya kiutumishi, atahitajika kuwasilisha barua ya
utambulisho kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora;
vi. Kwa mwombaji anayeomba pasipoti ya kidiplomasia atahitajika kuwasilisha
barua ya utambulisho kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki.
JINSI YA KUOMBA HATI YA DHARURA YA KUSAFIRIA
Ili kuomba Hati ya dharura ya Kusafaria mwombaji anatakiwa kufungua linki
ifuatayo:
http://etd.immigration.go.tz/etd_customer/
a. Baada ya kuingia katika ukurasa wa maombi ya shahada ya dharura, jaza
taarifa za mwombaji kwa usahihi na ukamilifu;
b. Ambatisha picha na viambato vinavyohitajika vya mwombaji;
c. Baada ya kukamilisha hatua zote chapisha fomu yako na uiwasilishe katika
Ofisi ya Uhamiaji iliyo karibu nawe (isipokuwa Ofisi ya Uhamiaji Kurasini na
Afisi Kuu Zanzibar). Ikiwa mwombaji yuko nje ya nchi, atawasilisha fomu
yake katika Ofisi ya Ubalozi;
d. Mara baada ya Afisa kujiridhisha na vielelezo na maelezo ya mwombaji,
atapatiwa Namba ya kumbukumbu ya malipo (control number) na atalipia
kiasi cha Tsh 20,000. Ikiwa yuko nje ya nchi atalipia dola 20;
e. Baada ya mwombaji kulipia, ombi lake litapokelewa na kufanyiwa kazi, na
mwombaji atapatiwa hati yake ndani ya masaa 24.
VIAMBATO VYA OMBI LA SHAHADA YA DHARURA
i. Cheti cha kuzaliwa mwombaji
ii. Cheti au kiapo cha kuzaliwa mmoja wa mzazi wa mwombaji au cheti cha
Tajnisi
iii. Kitambulisho cha Taifa (NIDA)
iv. Barua ya utambulisho toka Serikali ya Mtaa au Kijiji.
PASIPOTI IKIPOTEA AU KUIBIWA
Mwombaji akipoteza au kuibiwa pasipoti aliyopewa na akitaka kuomba pasipoti
nyingine atalazimika kuzingatia yafuatayo;
i. Atatakiwa kutoa taarifa polisi kuhusiana na uptevu au kuibiwa kwa pasipoti
yake.
ii. Atatangaza kwenye magazeti mawili moja la kiingereza na Kiswahili
kuhusiana na kuibiwa au kupteza pasipoti.
iii. Atatengeneza tamko la kusheria kuhusiana na upetevu wa pasipoti yake.
iv. Atajaza fomu ya maombi ya pasipoti nyingine kwa kufuata taratibu zote.
PASIPOTI IKIHARIBIKA
Ikiwa pasipoti itaharibika na mmiliki akawa anahitaji kupatiwa pasipoti nyingine
atazingatia mambo yafuatayo:
i. Atajaza fomu ya maombi mtandaoni;
ii. Atawasilisha barua ya maombi ya pasipoti nyingine inayoelezea mazingira
yaliyopelekea kuharibika kwa pasipoti yake ya awali;
iii. Atawasilisha pasipoti iliyoharibika wakati wa kuomba pasipoti nyingine.
KUTOA TAARIFA YA PASIPOTI ILIYOPOTEA AU KUIBIWA
Endapo mmiliki wa pasipoti atapoteza pasipoti yake au kuibiwa, anatakiwa kutoa
taarifa kwa maandishi katika Ofisi ya Uhamiaji iliyo karibu naye. Kwa wailiopoteza
pasipoti wakiwa nje ya nchi watatoa taarifa katika Ofisi ya Ubalozi. Aidha, mwombaji
anaweza kutoa taarifa ya upotevu kwa kupiga namba za simu zifuatazo:
+255 262-323542 au +255 262323532. Pia, taarifa hiyo inaweza kuwasilishwa
kupitia baruapepe ifuatayo:
lostpassport@immigration.go.tz
Taarifa muhimu zinazotakiwa kuripotiwa ni kama ifuatavyo:
i. Jina kamili la mmiliki wa pasipoti;
ii. Namba ya pasipoti (ikiwa anaikumbuka)’
iii. Tarehe na mahali ilipopotea;
iv. Sababu au mazingira yaliyopelekea upotevu
Aidha, mhusika ataripoti katika Kituo cha polisi ili kupatiwa Police Loss Report.
Mwombaji anayewasilisha ombi la pasipoti iliyopotea anaweza kupatiwa pasipoti
nyingine baada ya kuhojiwa na Afisa Mdhibiti wa Pasipoti kujiridhisha na mazingira
ya upoteaji
ADA MBALIMBALI ZA PASIPOTI NA HATI ZA SAFARI
Ada za Pasipoti na Hati za Safari ni kama zilivyo oneshwa kwenye jedwali hapa chini:
Aidha, unaweza kuzipata ada hizo moja kwa moja kutoka kwenye tovuti yetu
kupitia linki ifuatayo:
https://immigration.go.tz/index.php/application-fee-for-electronicpassports-and-travel-document
TAHADHARI
Pasipoti hii ni mali ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na inaweza
kuchukuliwa na Serikali wakati wowote. Ni hati ya thamani kubwa na hakuna ruhusa
ya kuibadilisha kwa namna yoyote au kuacha ichukuliwe na mtu yeyote asiyestahili
kuwa na Pasipoti hiyo. Kama ikipotea au kuharibiwa ni lazima taarifa kamili ipelekwe
mara moja kwenye Ofisi ya Uhamiaji, Kituo cha Polisi, Ubalozi wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ulio karibu au Ubalozi wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
MAWASILIANO
Ukiwa na tatizo katika kuomba pasipoti au Hati yoyote ya safari tafadhali wasiliana
nasi kupitia baruapepe ifuatayo:
info@immigration.go.tz AU
passporttanzania@immigration.go.tz
MAWASILIANO
Ukiwa na tatizo katika kuomba pasipoti au Hati yoyote ya safari tafadhali wasiliana
nasi kupitia baruapepe ifuatayo:
info@immigration.go.tz AU
passporttanzania@immigration.go.tz
13.1 ANUANI YA UHAMIAJI MAKAO MAKUU
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji,
Barabara ya Mwangosi,
S.L.P 1181,
Dodoma.
NUANI YA AFISI KUU ZANZIBAR
Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar,
S.L.P 1354,
Zanzibar.