Wosia wa mirathi ni hati rasmi au maelezo yaliyoandikwa ambayo mtu huacha ili kueleza jinsi mali yake itakavyogawanywa baada ya kifo chake. Katika Uislamu na sheria nyingi za kiraia, wosia ni nyaraka muhimu inayosaidia kuzuia migogoro ya familia na kuhakikisha haki inatekelezwa kulingana na matakwa ya marehemu.
Aina za wosia
Wosia wa mdomo
Huu ni wosia unaotolewa kwa maneno ya mdomo yaani ‘Oral will’. Japokuwa aina hii ya wosia ni ngumu wakati mwingine kuthibitishwa lakini sharia inautambua kuwa ni wosia kama vile ulivyo ule wa maandishi. Kwa mfano, Local Customary Law (Declaration) (No. 4) Order, 1963 inataka wosia huu ni lazima utolewe wakiwepo mashahidi wanne (4) yaani wawili wawe ni ndugu na wawili wasiokuwa ndugu. Mke au wake za marehemu, kama anaye au anao, ni lazima awe nyongeza ya mashahidi hao. Kigezo hiki kisipofuatwa basi wosia huo utabatilishwa kweupee.
Wosia wa maandishi
Huu ni wosia unaotolewa kwa njia ya maandishi. Wakati mwingine unajulikana kama wosia rasmi. Lengo lake ni sawa tu kama lilivyo la wosia wa mdomo kama nilivyoeleza hapo juu. Umakini wa hali ya juu sana unatakiwa uzingatiwe katika kuandika wosia huu.
Ni lazima ‘legal formality’ yaani matakwa ya kisheria yafuatwe wosia wa aina hii unaopoandikwa. Baadhi ya matakwa hayo ni kama vile ni lazima uwe kwa maandishi na kusainiwa na mtoa wosia huo mbele ya mashahidi, ushuhudiwe angalau na mashahidi wawili na ni vizuri mmoja kati yao akawa ni nduguye mtoa wosia; mashahidi hao wanaweza kuzidi wawili ila tu wasipungue.
Wosia wa maandishi unaweza ukabatilisha wosia uliotolewa awali kwa mdomo, isipokuwa wosia wa mdomo hauwezi kubatilisha ule wa maandishi. Na anayeweza kufanya hivyo ni mtoa wosia peke yake na si mtu mwingine.
3.Wosia wa masharti fulani
Unaweza ukauitwa ‘Conditional will’ ambapo masharti fulani aliyoyaweka mtoa wosia na ni lazima yatimizwe kwanza ndipo tunaweza kusema wosia una nguvu kisheria. Msharti haya yanatakiwa yawe ni yale yanayotekelezeka.
Kwa mfano mtoa wosia anaweza kusema nyumba hii apewe Comfort pindi atakapooa au atakapoweza kupata Shahada yake ya kwanza ya Sheria, hivyo basi ikiwa mtoa wosia huo amefariki nyumba hiyo haitokwenda kwa Comfort mpaka atakapokuwa ameoa au kupata Shahada yake ya kwanza ya Sheria.
Mambo ya msingi ya kuzingatiwa wakati wa kuandaa wosia
Wosia ni lazima uwe na mambo yafuatayo vinginevyo inaweza kupelekea ukabatilishwa na mpango wa kugawanya mali bila wosia ukachukua nafasi. Mambo hayo ni kama vile:
- Mtoa wosia ni lazima kisheria awe na uwezo wa kuacha wosia. Hapa nina maana ya kwamba sharia inahitaji mtu anayetoa wosia awe na umri wa miaka isiyopungua kumi na minane (18). Pia anatakiwa awe na akili timamu wakati wa kuacha wosia huo. Hali kadhalika mtu mwenye matatizo ya akili anaweza kuandika wosia pindi tatizo hilo limemwondoka kwa mfano endapo atakuwa anasumbuliwa na tatizo la ukichaa wa muda ‘temporary insanity’. Mtu akiwa na akili timamu na akaandika wosia lakini baadae akapata ukichaa wosia ule hautokuwa batili kwani wakati anauandika alikuwa na utimamu wa akili.
- Mtoa wosia ni lazima afahamu yale yaliyoandikwa katika wosia. Kwa mfano mwacha wosia kaandikiwa wosia eidha na wakili au mtu yeyote ni lazima afahamu yale yaliyoandikwa ndani kabla hajaweka saini.
- Wosia ni lazima utaje majina ya mtoa wosia.
- Wosia unatakiwa utaje atakaye simamia mirathi.
- Wosia ni lazima uwe na tarehe ya siku wosia huo ulipoandaliwa.
- Wosia ni lazima utaje aina na kiwango cha thamani ya mali zinazotolewa katika wosia. Kama kuna kitu kinamilikiwa na watu wawili au zaidi basi ni sharti hilo libainishwe katika wosia.
- Wosia unatakiwa utaje idadi ya warithi na wanufaika wa mirathi hiyo.
- Wosia unatakiwa utilie maanani vipi itakapotokea mrithi au warithi na mnufaika au wanufaika watakapofariki kabla ya mtoa wosia.
- Wosia unatakiwa utilie maanani ndoa inayoweza kufungwa baada ya wosia kuandaliwa. Ndoa itakayofungwa baada ya wosia kuandikwa inaweza kuathiri wosia huo.
- Wosia ni lazima usainiwe na mtoa wosia mbele ya mashahidi.
- Wosia ni lazima uthibitishwe na mashahidi.
- Mtoa wosia ni lazima aonyeshe ya kuwa ameandika wosia huo akiwa na akili timama pia bila kushurutishwa.
- Lazima katika wosia kuwe na kipengele kinachoonyesha ya kuwa mtoa wosia akibatilisha wosia wowote alioutoa awali.
- Endapo mtu ambaye kwa kawaida alitakiwa kupewa sehemu ya mirathi lakini hakutajwa katika wosia basi ni vyema sababu zikatolewa.
Endapo mambo haya yatazingatiwa itapunguza kwa kiasi kikubwa matatizo yanayoweza kutokea baadae mtoa wosia atakapokuwa amekwisha fariki, mfano, wosia huo kukataliwa au kubatilishwa kwa kutokufuata taratibu kama nilivyokwisha kuelezea kwa uchache hapo awali.
Muhimu: Ifahamike ya kwamba hakuna fomula maalumu ya kuandika wosia lakini endapo utazingatia mambo niliyoyataja hapo juu basi wosia wako utakuwa una nguvu kama wosia mwingine wowote.
Umuhimu wa Kuandika Wosia
- Kuzuia Migogoro ya Familia – Wosia ulio wazi husaidia familia kuepuka mabishano kuhusu mgawanyo wa mali.
- Kuhakikisha Haki ya Warithi – Unahakikisha kuwa warithi wanapata haki yao kulingana na sheria.
- Kutekeleza Matakwa Binafsi – Wosia unaweza kutaja matumizi maalum ya mali, kama kutoa misaada au kusaidia watu fulani.
- Kurahisisha Utaratibu wa Kisheria – Husaidia kupunguza changamoto zinazoweza kutokea katika ugawaji wa mali baada ya kifo.
Hatua za Kuandika Wosia wa Mirathi
1. Kuorodhesha Mali na Madeni
- Andika orodha ya mali zote unazomiliki, ikiwa ni pamoja na ardhi, nyumba, magari, akaunti za benki, na vitu vingine vya thamani.
- Tambua madeni yoyote unayodaiwa na utaje jinsi yatakavyolipwa kabla ya mgawanyo wa mali.
2. Kutaja Warithi
- Eleza ni nani atakayepokea mali na kwa kiasi gani.
- Ikiwa ni wosia wa Kiislamu, fuata taratibu za mirathi kama zinavyoelekezwa kwenye Qur’an (Surah An-Nisa, 4:11-14).
3. Kuteua Wasimamizi wa Mirathi
- Chagua mtu au watu wa kuaminika kusimamia mgawanyo wa mali.
- Wasimamizi hawa wanapaswa kuwa watu wenye uadilifu na wanaojua taratibu za mirathi.
4. Kuweka Maelekezo Maalum
- Ikiwa unataka kutoa sehemu ya mali yako kwa shughuli za hisani, eleza wazi kiasi na shirika husika.
- Eleza ikiwa kuna masharti yoyote kuhusu mali fulani (mfano: matumizi ya mali kwa watoto hadi wafikie umri fulani).
5. Kushuhudiwa kwa Wosia
- Katika Uislamu, wosia unapaswa kushuhudiwa na angalau mashahidi wawili waadilifu.
- Katika sheria za kiraia, inashauriwa wosia uwe na sahihi ya mtoa wosia na mashahidi.
6. Kuhifadhi Wosia Mahali Salama
- Hifadhi wosia mahali salama, kama ofisi ya wakili, benki, au sehemu nyingine ya usalama.
- Mtaarifu mtu wa karibu kuhusu mahali ulipouhifadhi.
Soma Hii :Jinsi ya kuandika talaka ya kiislamu
Ni nani anapaswa kuandika wosia?
Mtu yeyote, awe mwanaume au mwanamke, kijana au mzee, mwenye mali nyingi au chache, mwenye umri wa miaka kumi na minane (18) na kuendelea akiwa na akili timamu wakati wa kuacha wosia basi anakidhi vigezo vya kuacha wosia.
MFANO/SAMPO YA WOSIA
- Huu ni wosia wangu wa mwisho mimi ………………………………wa S.L.P…………………………………
- Namchagua ………………………………………………………………………….
wa S.L.P. ……………………………………………………………………………….
Simu………………………………………………………………………………………
ambaye anaishi …………………………………….kuwa msimamizi wa mirathi yangu.
- Nitakapokufa mwili wangu ukazikwe……………………………………………..
Wilaya ……………………………………Mkoa………………………………………
- Mali zangu ni:
(a)………………………………………………………………………………………
( b ) ……………………………………………………………………………………
( c )……………………………………………………………………………………..
( d ) Nina akaunti zifuatazo:…………………………………………………………
………………………………………………………………………………………….
- Natamka kwamba mali zangu zote zinazohamishika na zisizohamishika zitamilikiwa na mke/mume wangu aitwaye……………………………iwapo atakuwa hai baada ya kufa kwangu.
- Iwapo mke/ mume wangu aitwaye ……………………………………..atafariki mapema kuliko mimi , mali zangu zitarithiwa na watoto wangu wafuatao:-
(a)………………………………………………………………………………………….
S.L.P………………………………………………………………………………………
Simu…………………………………………………………………………………………
(b)……………………………………………………………………………………………
S.L.P…………………………………………………………………………………………
Simu………………………………………………………………………………………..
(c)………………………………………………………………………………………….
S.L.P…………………………………………………………………………………………
Simu………………………………………………………………………………………..
(d)……………………………………………………………………………………………
S.L.P………………………………………………………………………………………….
Simu ………………………………………………………………………………………….
Katika mafungu yaliyo sawasawa ( kama si katika mafungu sawa utaainisha mbele ya kila jina la mtoto/mrithi kile ulichompa ) .
Imetiwa saini hapa……………………………………………….……….………………….
Siku ya………..…………………………………………………………………………………
Mwezi wa………….…………………mwaka………………………………………………
Saini ya mwosia…………….………………………………………………….……………
Shahidi wa Kwanza:
Jina:…………………………….………………………………………………………………..…….
Saini:…………………………………………………………….………………………………………
Anuani:………………………………………………………………………………………………
Kazi…………………………………………………………………………………………………..
Shahidi wa Pili :
Jina:………………………………………………………………………………………………….
Saini:…………………………………………………………………………………………………
Anuani:………………………………………………………………………………………………
Kazi…………………………………………………………………………………………………..
Mbele ya …………………………………………………………………………………………….
………………………………………………………………………………………………………….
WAKILI
Mshuhudi viapo/Saini:……………………………………………………………………………….
ANGALIZO: Watu wengi kutokana na athari za kiimani au tamaduni huhisi kuandika wosia ni kujichuria Laa hasha si kweli kabisa Bali kuandika wosia ni kuepusha migogoro isiyo ya lazima Baada ya kifo chako dhidi ya Mgawanyo na Usimamizi wa mali ulizoziacha.

