Genital Warts ni mojawapo ya magonjwa ya zinaa yanayosababishwa na virusi vya Human Papillomavirus (HPV). Ugonjwa huu husababisha uvimbe mdogo au vinyama laini vinavyoota kwenye sehemu za siri za mwanamke au mwanaume. Ni ugonjwa wa kawaida unaoathiri watu wengi ulimwenguni, hasa wale walio na maisha ya ngono yasiyo salama.
Ugonjwa huu husambazwa kwa mgusano wa ngozi kwa ngozi hasa wakati wa ngono, japo migusano mingine ya maeneo athirika isiyohusisha ngono inaweza pia kuwa chanzo cha kusambaa kwake.
Virusi wanaosababisha ugonjwa huu huwa na uhusiano wa moja kwa moja na kutokea kwa saratani ya mlango wa kizazi, saratani ya koo, uke, uume pamoja na saratani ya njia ya haja kubwa, hivyo ni vyema wagonjwa wakatibiwa haraka na kwa usahihi ili kuepusha changamoto hizi.
Mara baada ya kuambukizwa, ugonjwa huu huweza kuchukua mpaka muda wa wiki sita hadi miezi 6 kwa masundosundo kuwa dhahiri, ingawa baadhi ya wagonjwa wanaweza kukaa hata miaka kadhaa bila kuwa na dalili yeyote ile.
Kisababishi Cha Ugonjwa Wa Genital Warts:
Ugonjwa wa genital warts husababishwa na virusi wajulikanao kwa kitaalamu kama Human papilloma virus (HPV).
Ripoti ya shika la afya duniani (WHO) zinasema kwamba kuna aina zaidi ya 100 ya virusi wa papilloma waliokwisha kugunduliwa mpaka sasa ambapo kati ya hao ni aina mbili tu, HPV-6 na HPV-11 ambao ndio husababisha genital warts.
Kumbuka: Tafiti kadhaa zimeonesha kuwa baadhi ya aina za virusi wa HPV pia husababisha saratani ya shingo ya kizazi (carcinoma of the cervix) kwa wanawake au saratani ya njia ya haja kubwa (anal cancer) kwa jinsia zote mbili. Aina hii ya virusi hujulikana pia kama high-risk HPV.
Tabia Hatarishi Zinazoweza Kukupelekea Kupata Genital Warts.
- Kufanya ngono isiyo salama na mtu aliyeathirika na HPV: Ni muhimu kutumia kinga kama condoms ili kuzuia maambukizi, hii ni muhimu sana kwa wale wenye wapenzi wengi au wanaojihusisha na ngono kupita kiasi.
- Oral sex, au ngono kupitia mdomo: kufanya ngono kwa kutumia mdomo inakuweka katika hatari ya kupata warts au kuota vinyama sehemu za mdomo.
- Ngono katika umri mdogo: Watu wanaoanza ngono mapema wapo kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata genital warts kutokana na kinga za mwili kua chini sana.
Dalili Za Ugonjwa Wa Genital Warts:
Ugonjwa wa genital warts huonekana kama vioteo laini vinavyojitokeza juu ya ngozi ingawa wakati mwingine vinaweza kuwa vidogo mno kiasi cha kutoweza kuonekana vizuri kwa macho ya kawaida.
Kwa wanaume, vioteo hivi hutokea zaidi kwenye uume, ngozi ya pumbu, eneo la mitoki, mapajani pamoja na maeneo ya kuzunguka nje ya njia ya haja kubwa au ndani yake; wakati kwa wanawake hutokea ndani ya uke au njia ya haja kubwa, nje ya uke au ngozi ya nje kuzunguka njia ya haja kubwa, au ndani ya uke kuzunguka eneo la shingo ya kizazi.
Kwa wale wanaopenda kufanya ngono ya mdomoni (oral sex), wanaweza kupatwa na masundosundo/genital warts kwenye maeneo ya kuzunguka mdomo (lips), kwenye ulimi na hata kwenye utando unaozunguka koo.
Dalili nyingine ya ugonjwa wa genital warts ni kama vile mgonjwa kujihisi kukosekana kwa hisia (kufa ganzi) maeneo yaliyozungukwa na masundosundo.
kwa wanawake kuongezeka kwa utoko/ uchafu sehemu za siri, kuwashwa sana maeneo ya siri na wakati mwingine kutokwa na damu ukeni mara baada ya tendo la ngono. Hata hivyo dalili hizi hutokea mara chache sana.
Wanawake wengi vijana wanaojihusisha na vitendo vya ngono [sexually active] huambukizwa sana ugonjwa huu lakini wengi wao hupona bila hata kuhitaji matibabu, wakati wanaume wanaoambukizwa, wengi wao huwa hawaoneshi dalili zozote za ugonjwa ingawa wanaweza kuwaambukiza wenzi wao bila ya wao kujua.
Matibabu Ya Ugonjwa Wa Genital Warts:
Ni vema genital warts zitibiwe hospitali na daktari, haishauriwi kutumia dawa za kununua kujitibu mwenyewe kwa vile kuna uwezekano mkubwa wa kuchanganya aina ya dawa zinazotumika maalum kutibu aina nyingine za warts kwa ajili ya kujitibu genital warts.
Matibabu ya genital warts hufanyika hospitali kwa kuondoa vioteo juu ya ngozi iliyoathirika au kwa kutumia dawa utakazoandikiwa na daktari na kuelekezwa namna ya kuzitumia mwenyewe nyumbani kwa siku kadhaa mpaka majuma kadhaa. Dawa zinazotumika ni pamoja na Podophyllin na podofilox, Trichloroacetic acid (TCA) au Imiquimod.
Jinsi Ya Kutumia Podophyllin:
Chukua kiasi kidogo cha podophyllin cream, paka kwenye genital warts kwa kutumia pamba safi, subiri podophyllin cream ikae kwenye genital warts angalau kwa muda wa saa1 mpaka masaa 4 baada ya hapo osha eneo lilioathiriwa na genital warts kwa kutumia maji safi. Rudia hayo matibabu kila wiki kwa muda wa wiki nne mpaka wiki sita au mpaka pale genital warts zitakapokuwa zimeondoka kabisa.

Ukiachilia mbali matumizi ya dawa, masundosundo yanaweza pia kutibiwa kwa njia ya upasuaji mdogo kama vile kwa kuvikata, au kuvimaliza kwa kutumia njia ya baridi/barafu (Cryosurgery), njia ya umeme (Electrocauterization) au kuvikausha kwa kutumia mionzi maalum ya laser (Laser therapy).

Matibabu ya masundosundo, kama yalivyo matibabu ya magonjwa mengine yanayosambaa kwa njia ya ngono, ni lazima yahusishe pia tiba kwa mwenza wa mgonjwa. Wakati mwingine hata kama utajihisi huna dalili za waziwazi, ni vema kumuona daktari ili uchunguzwe na kutibiwa kuepusha kusambaza ugonjwa kwa watu wengine au kuachia ugonjwa mpaka ukakuletea madhara zaidi.
Aidha matibabu yanaweza kuhitaji kurudiwa rudiwa mara kadhaa mpaka masundosundo yatakapokuwa yametoweka kabisa.
Kwa wanawake ambao wametibiwa genital warts na kupona au wale ambao wamewahi kuwa na wenza waliowahi kuugua ugonjwa huu, wanashauriwa sana kufanya uchunguzi wa mara kwa mara wa shingo za kizazi (pap smear). Kwa wanawake waliowahi kuugua genital warts, ni vema kufanya pap smear walau kila baada ya miezi 3 mpaka 6 tangu kupata matibabu ya awali ya genital warts.

Madhara Ya Ugonjwa Wa Genital Warts:
Kwa baadhi ya wagonjwa, masundosundo yanaweza kuwa mengi na makubwa sana kiasi cha kuhitaji matibabu ya muda mrefu na ghali zaidi pamoja na ufuatiliaji wa kina.
Jinsi Ya Kujikinga Na Ugonjwa Wa Genital Warts:
Njia mojawapo ya uhakika kabisa ya kujiepusha na ugonjwa wa genital warts pamoja na magonjwa mengine ya ngono/zinaa ni kujiepusha na matendo ya ngono na zinaa kabisa.
Lakini kwa wale ambao ni ngumu kufanya hivyo, wanaweza kupunguza uwezekano wa kupatwa na ugonjwa huu kwa kujihusisha kingono na mwenza mmoja tu ambaye una uhakika kuwa hajaambukizwa wala hayupo katika hatari ya kuambukizwa magonjwa haya.
Tofauti na magonjwa mengine ya zinaa, matumizi ya condom hayana uhakika wa asilimia mia moja katika kukukinga dhidi ya HPV kwa sababu virusi wa HPV au hata masundosundo yanaweza kuwa nje kwenye ngozi ambayo uwezekano wa kugusana ni mkubwa.
Pamoja na hayo, bado condom inaweza sana kupunguza hatari ya kuambukizwa masundosundo ikiwa tu itatumika vema na inashauriwa kuitumia mara zote unapokutana kingono na mwenza usiye na uhakika naye. Tukumbuke kila wakati kuwa HPV inaweza bado kuambukizwa kwa mtu hata kama mwenza hana masundosundo yanavyoonekana au hana dalili zozote zile.
Ikiwa kuna uwezekano, ni vyema kwa wanawake wote wenye umri wa miaka kati ya 9 mpaka 26 kupata chanjo dhidi ya virusi wa HPV ili kuzuia uwezekano wa kuambukizwa virusi hao ambao hatimaye husababisha saratani ya shingo ya kizazi.