Mamlaka ya Mapato Tanzania -TRA Wametangaza Tarehe Rasmi ya kutangaza Matokeo ya Usaili wa kuandika Uiofanyika kuanzia March 29 mpaka April 5 nchi nzima.
Akizungumzia mchakato huo leo Jumatano Aprili 2, 2025 Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali watu na Utawala, Moshi Kabengwe amesema baada ya majina kutangazwa usaili wa vitendo na mahojiano utafuata.
Kabengwe amesema usaili wa vitendo utaanza Mei 2, 2025 hadi 4 kwa kada ya madereva na waandishi waendesha ofisi, huku usaili wa mahojiano kwa kada nyingine utafanyika kuanzia Mei 7 hadi 9.
Pia, ameeleza kuwa watakaofanikiwa kupita katika hatua hiyo wataarifiwa Mei 18, 2025 na kuanza mafunzo elekezi Mei 22 hadi Juni 2, 2025 watakapoajiriwa na kuanza kazi rasmi.
“Katika mchakato wa usaili maombi yaliyokidhi vigezo yalikuwa 112,952 yakaongezeka maombi 71 baada ya kukata rufaa na kufikisha idadi ya maombi 113,023 yaliyohusisha waombaji 86,314 na waliofanya usaili wa maandishi ni waombaji 78,544 sawa na asilimia 91 ya waombaji wote.
“Waombaji 7,770 sawa na asilimia 9 hawakufika kwenye usaili kwa sababu mbalimbali. Sera ya TRA ni ajira sawa kwa wote na zilizotangazwa zitazingatia sifa na vigezo vya muomba kazi bila kujali hali ya muhusika kwamba ni mtoto wa maskini, wa kiongozi au wa mtumishi wa umma, ndiyo maana vituo vya usaili viliwekwa kwenye mikoa minane na Zanzibar ili kusogeza huduma karibu,”amesema na kuongeza Kabengwe
Ikumbukwe kuwa
Mamlaka ya Mapato Tanzania ilitangaza nafasi za kazi kuanzia tarehe 6 hadi 19 Februari, 2025, ambapo tarehe 21 Machi, 2025 Mamlaka ilitoa taarifa kwa umma kwamba baada ya kufunga zoezi la kupokea jumla ya maombi 135,027 yalipokelewa.
Soma Hii : Maswali ya Usaili TRA Written na Oral
Kati ya maombi hayo, maombi 112,952 yalikidhi vigezo vya kuitwa kwenye usaili wa kuandika na tarehe 23 Machi, 2025 Mamlaka ilitoa fursa ya siku mbili (24 na 25 Machi, 2025) kwa waomba kazi ambao walidhani walistahili kuitwa kwenye usaili wa kuandika ila hawakuitwa na baada ya kutolewa kwa fursa hiyo jumla ya maombi 71 yalikidhi vigezo na hivyo kufanya jumla ya maombi 113,023 kukidhi vigezo vya kufanya usaili wa kuandika.