Kisonono ni mojawapo ya magonjwa ya zinaa yanayoenea kwa kasi duniani kote. Ugonjwa huu husababishwa na bakteria aitwaye Neisseria gonorrhoeae. Kisonono huathiri zaidi mfumo wa uzazi, lakini pia unaweza kuathiri sehemu nyingine za mwili kama koo, macho na puru (mkundu), hasa kwa watu wanaojihusisha na aina mbalimbali za ngono.
Maana ya Kisonono
Kisonono ni ugonjwa wa bakteria unaoambukizwa kupitia ngono isiyo salama. Ni kati ya magonjwa ya zinaa yanayoenea kwa haraka zaidi, na unaweza kuambukizwa kwa njia ya:
Ngono ya ukeni, mdomoni au puru bila kutumia kondomu
Kugusana na majimaji ya sehemu za siri za mtu aliyeambukizwa
Kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua
Dalili za Kisonono
Kwa Wanaume:
Kutokwa na majimaji meupe au ya kijani kutoka kwenye uume
Maumivu au hali ya kuchoma wakati wa kukojoa
Kuvimba kwa korodani au maumivu ya korodani
Kujikuna sehemu za siri
Maumivu wakati wa tendo la ndoa
Kwa Wanawake:
Kutokwa na uchafu usio wa kawaida ukeni
Maumivu wakati wa kukojoa
Maumivu ya tumbo la chini
Maumivu wakati wa tendo la ndoa
Kutokwa na damu isiyo ya hedhi
Kuwashwa au kuvimba ukeni
NB: Mara nyingine mtu anaweza kuwa na kisonono bila dalili yoyote, hali inayoongeza hatari ya kuusambaza bila kujua.
Madhara ya Kisonono Usipotibiwa
Ugumba kwa wanawake na wanaume
Maambukizi ya kizazi (PID – Pelvic Inflammatory Disease)
Maumivu sugu ya nyonga
Mimba ya nje ya kizazi
Kuambukiza mtoto wakati wa kujifungua (mtoto anaweza kuwa kipofu)
Kuongezeka kwa hatari ya kupata au kusambaza virusi vya UKIMWI (HIV)
Tiba ya Kisonono
Kisonono hutibiwa kwa kutumia antibiotiki. Dawa zinazotumika ni:
1. Ceftriaxone
Huchomwa kwenye msuli (sindano)
Mara nyingi hutolewa pamoja na dawa ya kumeza kama azithromycin
2. Azithromycin au Doxycycline
Dawa za kumeza zinazosaidia kuua bakteria wote walioko mwilini
Tahadhari:
Usijitibu mwenyewe bila maelekezo ya daktari
Maliza dozi yote hata kama dalili zimepotea
Hakikisha mwenzi wako pia anatibiwa
Jinsi ya Kujikinga na Kisonono
Tumia kondomu kila unapofanya ngono
Pima afya mara kwa mara, hasa ukiwa na mwenzi mpya
Epuka kuwa na wapenzi wengi
Kuwa mwaminifu kwenye uhusiano
Epuka ngono ya mdomoni au puru bila kinga
Wajawazito wapaswa kupima mapema ili kuepusha maambukizi kwa mtoto
Maswali Yaulizwayo Mara kwa Mara (FAQs)
Kisonono ni ugonjwa wa aina gani?
Ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria aina ya *Neisseria gonorrhoeae* na huambukizwa kwa ngono isiyo salama.
Dalili za kisonono huanza baada ya muda gani?
Dalili huweza kuanza kati ya siku 2 hadi 7 baada ya kuambukizwa.
Je, kisonono kinaweza kupona bila dawa?
Hapana. Kisonono kinahitaji tiba ya antibiotic kutoka kwa daktari. Bila tiba kinaweza kusababisha madhara makubwa.
Kisonono kinaweza kuambukiza kwa busu au kushikana mikono?
Hapana. Kinaambukizwa kupitia ngono au kugusana na majimaji ya sehemu za siri.
Je, mtoto anaweza kuambukizwa kisonono?
Ndiyo, kupitia kujifungua kama mama ameathirika. Mtoto anaweza kupata maambukizi ya macho.
Ni dawa gani hutibu kisonono?
Ceftriaxone, Azithromycin na Doxycycline ni dawa maarufu za kutibu kisonono.
Je, mtu anaweza kupata kisonono mara ya pili?
Ndiyo. Ukifanya ngono tena na mtu aliyeambukizwa unaweza kuambukizwa upya.
Kisonono ni hatari kwa wanaume tu?
Hapana. Ni hatari kwa jinsia zote na huleta madhara kwa wanawake na wanaume endapo haitatibiwa.
Je, kisonono kinaweza kuathiri mimba?
Ndiyo. Kinaweza kusababisha mimba kutoka, uchungu mapema au mtoto kuzaliwa na maambukizi.
Je, kisonono huathiri uzazi?
Ndiyo. Kinaweza kuharibu mirija ya uzazi kwa wanawake na kusababisha ugumba.
Je, kuna chanjo ya kisonono?
Kwa sasa, hakuna chanjo ya kuzuia kisonono. Njia bora ni kinga na kupima mara kwa mara.
Kisonono huathiri sehemu zipi za mwili?
Uume, uke, puru, koo na hata macho, hasa kwa wanaofanya ngono ya mdomo au puru.
Kisonono kinaweza kuchukua muda gani kupona?
Kwa tiba sahihi, dalili hupungua ndani ya siku chache, lakini kupona kabisa huchukua siku 7–14.
Je, mtu akitibiwa anaweza kuambukiza tena?
Hapana, ikiwa amepata tiba kamili. Lakini anaweza kuambukizwa tena kutoka kwa mtu mwingine.
Je, unaweza kuwa na kisonono na usijue?
Ndiyo. Kisonono mara nyingine hakioneshi dalili, hasa kwa wanawake.