Mafuta halisi ya nazi unaweza ukayatengeneza ukiwa nyumbani kwako ili kupunguza gharama za kununua mafuta ya Brand za watu ,Makala hii itakupa muongozo jinsi ya kutayarisha mafuta ya Nazi.
Vitu Muhimu vya Kutayarisha
1, Nazi yako iwe safi na nzima sio mbovu
Andaa sufuria yako kwa ajili ya kupikia mafuta jikoni, hakikisha una ‘blenda’ au kibao cha mbuzi kwa ajili ya kukunia nazi ili uweze kupata tuwi la nazi.
2, Uwe na Chujio kwa ajili ya kuchuja machicha ya nazi na kuweza kupata tuwi haliyakuwa safi kabisa. Andaa jiko lenye moto ambalo litatumika kwa ajili ya kuchemsha mafuta ili yaweze kujitenga na maji.
Jinsi ya kuandaa Mafuta ya Nazi
Anza kwa kuandaa nazi, kwa kuzikuna kwa kutumia kibao au kuzisaga kwa blenda mpaka zitakapokuwa laini.
Endelea kwa kuchuja nazi kwa maji masafi ili kuhakikisha unapata tui zito la kutosha ambalo utaweza kupata mafuta kwa wingi zaidi.
Baada ya kuchuja weka tui katika chombo kisafi na uliache kwa masaa 12 au zaidi. Unaweza kuweka katika friji au sehemu yoyote yenye joto la wastani.
Ili kufahamu kama tui lipo tayari kwa hatua inayofuata utaona limejitenga kwa kutengeneza matabaka mawili la juu likiwa limeganda au kushikana kiasi na chini likiwa maji matupu.
Ukifikia hapo tumia chujio kuondoa maji na ubaki na tui zito lililoganda kwa ajili ya kuendelea na hatua nyingine.
Endelea kwa kuwasha jiko na kubandika sufuria yenye tui jikoni kisha uache lichemke hadi litakapoanza kutoa mafuta.
Baada ya hapo chuja mafuta kwa chujio au kitambaa kisafi kuondoa makapi yaliyopatikana kisha utayahifadhi katika chombo kisafi kwa ajili ya matumizi.
Mapaka hapo utakuwa tayari umetengeneza mafuta mazuri ya nazi, unaweza kuongeza viungo kama majani au mafuta ya ‘rosemary’ ili kuongeza harufu nzuri.