Maumivu ya jino ni moja ya maumivu mabaya sana kuyapata, maumivu mengine mabaya zaidi ni maumivu ya sikio.
Jino linaweza kupatwa na maumivu ambayo yanaweza kupelekea jino kutoboka na hata kuong’olewa kabisa.
Maumivu haya yanaweza kuletwa na maambukizi ya bakteria kutokana na vyakula tunavyokula au kutokusafisha kinywa vizuri kila siku, jino kupata jeraha, magonjwa ya fizi, na udhaifu wa mifupa mwilini mwako kwa ujumla.
Maumivu mengi ya jino ni ishara kuwa huna chumvi ya kutosha mwilini, huna maji ya kutosha mwilini na hujishughulishi na mazoezi ya viungo kila mara.
Dawa 8 zifuatazo zinaweza kutuliza maumivu ya jino na hata kuliziba kabisa iwapo tayari limeanza kutoboka.
1. Asali yenye mdalasini
Chukua asali vijiko vidogo vitatu na uchanganye na mdalasini ya Unga kijiko kikubwa kimoja. Pakaa mchanganyiko huu kidogo kidogo juu ya jino linalouma kutwa mara 3.
2. Aloe vera (mshubiri)
Pata aloe vera fresh na uchane kupata maji maji yake (utomvu) na unyunyize juu ya hilo jino linalouma kidogo kidogo kutwa mara 2.
3. Mafuta ya nazi na karafuu
Chukua karafuu 3 zitwangwe kwenye kinu, changanya na mafuta ya asili ya nazi kijiko kidogo kimoja uliyotengeneza mwenyewe nyumbani. Pasha kwenye moto kama dakika tatu, ipua na usubiri mchanganyiko wako upoe.
Paka mchanganyiko huu juu ya jino linalouma na uache kwa dakika 7 kisha jisukutue kinywa na maji.
4. Majani ya mpera
Majani freshi ya mti wa mpera yanatibu pia jino linalouma sababu ya sifa yake ya kutibu maambukizi na huua pia bakteria wabaya wanaoshambulia jino.
Tafuna tu jani moja au mawili ya mti huu mpaka mara mbili kwa siku kwa siku kadhaa na jino litaaacha kuuma.
Unaweza pia kuchemsha katika moto majani kadhaa ya mti huu kisha ipua chuja na uongeze chumvi kidogo ya mawe ya baharini na utumie kusafishia kinywa chako ukitumia mswaki mara 2 kwa siku kwa siku kadhaa.
5. Maji ya uvuguvugu na chumvi
Mchanganyiko rahisi wa maji ya uvuguvugu na chumvi unaweza kusaidia kutibu maumivu ya jino.
Changanya nusu kijiko cha chai cha chumvi ya mawe ya baharini na maji ya uvuvugu glasi moja na utumie kusafisha kinywa chako ukitumia mswaki mara 2 kwa siku kwa siku kadhaa.
Mchanganyiko huu husaidia kutibu bakteria, maambukizi na uvimbe katika fizi.
6. Kitunguu maji
Kitunguu maji kina sifa ya kuzuia vijidudu nyemelezi ndani ya mwili na kinaweza kutumika pia kutibu maumivu ya jino kwa kuviua vijidudu vinavyosababisha kuoza kwa meno.
Tafuna silesi kadhaa cha kitunguu maji freshi ili kupunguza maumivu ya jino. Au kama huwezi kukitafuna basi weka tu kipande cha silesi cha kitunguu maji juu ya jino linalouma kwa dakika 10 hivi mara kadhaa kwa siku ili kuondoa hayo maumivu.
7. Kitunguu swaumu
Kutumia kitunguu swaumu pia kunaweza kurahisha kwa haraka kuondoa maumivu ya jino. Kitunguu swaumu huua bakteria, huua virusi pia ni antibiotiki ya asili isiyo na madhara kama antibiotiki za viwandani.
Tafuna punje 1 au 2 za kitunguu swaumu kila siku. Au katakata vipande vidogo vidogo vya punje 2 au 3 za kitunguu swaumu uchanganya na chumvi kidogo ya baharini kwa mbali na uweke mchanganyiko huo moja kwa moja juu ya jino linalouma na uache kwa dakika 5 au 7 hivi mara 2 kwa siku kwa siku kadhaa.
8. Pilipili na chumvi
Pilipili na chumvi unaweza kuwa mchanganyiko mzuri sana wa dawa za asili kwa kutibu maumivu ya jino sababu vyote viwili chumvi na pilipili hudhibiti bakteria na maambukizi mbalimbali.
Pata pilipili manga nyeupe au nyeusi ya unga na uchanganye kiasi sawa cha pilipili na chumvi ya mawe ya baharini kisha ongeza kiasi kidogo cha maji kupata uji mzito kidogo na uuweke juu ya jino linalouma kwa dakika kadhaa kila siku kwa siku kadhaa.
Epuka vyakula vitamu sana vya madukani, ice cream, pipi, na soda zote na vingine vya jamii hiyo.
Ni muhimu pia kuonana na daktari wa meno kwa uchunguzi zaidi kwani wakati mwingine dawa hizi zinaweza zisikuponye tatizo la jino kuuma au kutoboka kama unavyotarajia.
Sehemu nyingi mijini zipo kliniki maalumu kwa ajili ya meno tu, waone madaktari hao kwa uchunguzi juu ya matatizo yako ya meno mara kwa mara.