Kaswende (Syphilis) ni mojawapo ya magonjwa ya zinaa (STI) yanayoambukizwa kwa njia ya ngono na husababishwa na bakteria aitwaye Treponema pallidum. Ikiwa haitatibiwa mapema, kaswende inaweza kusababisha madhara makubwa ya kiafya ikiwemo matatizo ya moyo, ubongo, macho na hata kifo. Habari njema ni kwamba kaswende hutibika kabisa kwa dawa zinazopatikana hospitalini.
Dawa ya Kaswende: Tiba Iliyothibitishwa Kisayansi
1. Penicillin G Benzathine (Benzathine penicillin G)
Hii ndiyo dawa kuu na inayopendekezwa zaidi kwa matibabu ya kaswende. Dawa hii hutolewa kwa njia ya sindano kwenye msuli (intramuscular injection).
Hatua ya awali (Primary, Secondary au Early Latent):
Dozi moja ya sindano ya Benzathine Penicillin G (2.4 million units).Hatua ya latent ya muda mrefu (Late Latent au Unknown Duration):
Sindano 3 (kila moja 2.4 million units) zinazotolewa kwa wiki 3 mfululizo.Kwa wajawazito:
Penicillin ndiyo dawa pekee salama na bora kwa wajawazito. Ikiwa mama mjamzito ana aleji ya penicillin, tiba mbadala haifai — badala yake atahitaji desensitization na kutibiwa na penicillin.
2. Dawa Mbadala kwa Wale Walio na Aleji ya Penicillin
Kwa watu wasio na ujauzito lakini wana aleji ya penicillin:
Doxycycline (100mg mara 2 kwa siku kwa siku 14)
Tetracycline (500mg mara 4 kwa siku kwa siku 14)
Ceftriaxone (dozi tofauti kulingana na hali ya mgonjwa – hutolewa kwa sindano)
NB: Dawa hizi siyo bora kama penicillin, na hazifai kwa wanawake wajawazito.
Vipengele Muhimu Kabla ya Kuanza Matibabu
Upimaji wa damu (VDRL/RPR): Unasaidia kuthibitisha uwepo wa kaswende na hatua ya maambukizi.
Ushauri wa kitabibu: Daktari ataamua dawa sahihi kulingana na hatua ya ugonjwa, historia ya afya, na iwapo mgonjwa ni mjamzito.
Kupima magonjwa mengine: Mara nyingi kaswende huambatana na magonjwa mengine ya zinaa kama UKIMWI, hivyo kipimo kamili ni muhimu.
Je, Baada ya Tiba Unakuwa Umepona Kabisa?
Ndiyo, lakini:
Unahitaji kufuatiliwa kwa vipimo vya damu ili kuhakikisha maambukizi yametoweka.
Kutotibiwa ipasavyo au kukatisha dawa hupelekea kaswende kurudi au kusambaa zaidi.
Mgonjwa anapaswa kuacha kabisa tendo la ndoa hadi daktari athibitishe kuwa amepona.
Mambo ya Kuzingatia Wakati wa Matibabu ya Kaswende
Kumaliza dozi yote ya dawa kama ulivyoelekezwa.
Kuwashauri wapenzi wako wapimwe na kutibiwa pia.
Kuepuka ngono hadi upone kabisa.
Kufanya vipimo vya ufuatiliaji kwa muda uliopendekezwa na daktari.
Kudumisha usafi na afya ya mfumo wa uzazi.
Dawa za Asili au Mitishamba kwa Kaswende: Je, Zinafaa?
Mpaka sasa, hakuna dawa ya asili wala mitishamba iliyothibitishwa kisayansi kutibu kaswende. Kuweka matumaini kwenye dawa hizo kunaweza kuchelewesha matibabu sahihi na kusababisha madhara makubwa. Ni muhimu kutafuta matibabu ya kitaalamu hospitalini.
Maswali na Majibu Kuhusu Dawa ya Kaswende
Je, kaswende inatibika kabisa?
Ndiyo. Ikiwa utapata matibabu mapema kwa kutumia dawa sahihi kama penicillin, unaweza kupona kabisa.
Dawa bora ya kaswende ni ipi?
Penicillin G Benzathine ndiyo dawa bora na inayopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Naweza kutumia doxycycline badala ya penicillin?
Ndiyo, lakini ni kwa watu wasiokuwa wajawazito na walio na aleji ya penicillin.
Dawa za mitishamba zinaweza kutibu kaswende?
Hapana. Hakuna ushahidi wa kisayansi kuwa dawa za mitishamba zinatibu kaswende.
Je, kaswende inaweza kurudi baada ya matibabu?
Ndiyo, hasa kama mtu atafanya ngono na mwenza ambaye haja tibiwa.
Je, ninaweza kupata kaswende mara ya pili?
Ndiyo. Kupona kaswende hakukupi kinga ya maisha. Unaweza kuambukizwa tena.
Baada ya matibabu, ningoje muda gani kabla ya kufanya ngono?
Subiri hadi daktari athibitishe kuwa umepona kabisa kupitia vipimo vya damu.
Je, penicillin inapatikana kwenye zahanati za kawaida?
Ndiyo, penicillin hupatikana katika hospitali na zahanati nyingi za serikali au binafsi.
Je, naweza kunywa penicillin badala ya sindano?
Kwa kaswende, sindano ndiyo njia bora. Penicillin ya kumeza haifanyi kazi vizuri kwa aina hii ya maambukizi.
Je, ninaweza kujitibu kaswende bila kwenda hospitali?
Hapana. Unapaswa kwenda hospitali ili upate vipimo sahihi na tiba inayofaa.
Je, kaswende huathiri uwezo wa kupata watoto?
Ikiwa haitatibiwa kwa muda mrefu, inaweza kuharibu mfumo wa uzazi.
Ni mara ngapi nipime kaswende?
Angalau mara moja kwa mwaka, au kila baada ya kuwa na mpenzi mpya.
Je, mtu anaweza kuwa na kaswende bila dalili?
Ndiyo. Watu wengi huweza kuwa na kaswende katika hatua ya siri bila kujua.
Kwa nini kaswende ni hatari kwa wajawazito?
Inaweza kuambukiza mtoto tumboni na kusababisha madhara makubwa au kifo.
Penicillin inachukua muda gani kuponya kaswende?
Dalili huanza kuisha ndani ya siku chache, lakini vipimo vinaweza kuonyesha nafuu ndani ya wiki kadhaa.
Je, napaswa kurudia sindano ya penicillin?
Inategemea hatua ya ugonjwa. Daktari ndiye atakayeamua idadi ya sindano.
Je, kaswende inaweza kuwa sugu kwa dawa?
Mpaka sasa, hakuna ushahidi kuwa bakteria wa kaswende wamekuwa sugu kwa penicillin.
Mgonjwa wa kaswende anapaswa kufuata lishe maalum?
Lishe bora husaidia mwili kupona haraka, lakini hakuna chakula kinachotibu kaswende peke yake.
Je, kuna madhara ya penicillin?
Madhara madogo ni pamoja na maumivu kwenye sehemu ya sindano, homa au vipele. Madhara makubwa hutokea kwa walio na aleji.
Naweza kunyonyesha mtoto wangu nikiwa natibiwa kaswende?
Ndiyo, lakini mpeleke mtoto kupimwa kama kuna uwezekano aliambukizwa.

