Mkanda wa jeshi ni ugonjwa wa ngozi unaosababishwa na virusi vinavyojulikana kama Varicella-Zoster virus, virusi hivyo hivyo vinavyosababisha tetekuwanga. Baada ya mtu kuugua tetekuwanga, virusi hivyo hubaki ndani ya mwili vikiwa vamelala, na vinaweza kuamka baadaye na kusababisha mkanda wa jeshi (kwa Kiingereza huitwa shingles).
Ugonjwa huu huathiri zaidi watu wenye umri wa kati na wazee, au wale walio na kinga dhaifu. Hushambulia upande mmoja wa mwili, mara nyingi sehemu ya kifua, mgongo au uso.
Dalili za Ugonjwa wa Mkanda wa Jeshi
Dalili za awali huanza kabla ya vipele kuonekana. Dalili hizi huweza kujitokeza kwa muda wa siku 1 hadi 5 kabla ya madoa na malengelenge kuonekana:
Dalili za awali:
Maumivu au kuwashwa sehemu fulani ya mwili (hasa upande mmoja)
Hisia za kuchoma au kuchokozwa kwenye ngozi
Homa ya mwili
Uchovu na maumivu ya misuli
Maumivu ya kichwa
Kichefuchefu
Baada ya siku chache:
Madoa mekundu hutokea kwenye ngozi
Hutengeneza malengelenge yenye maji
Malengelenge hukauka na kuacha makovu
Maumivu makali yanayoweza kudumu hata baada ya vipele kupona (Postherpetic Neuralgia)
Sehemu Zinazoathiriwa Zaidi
Kifua na mbavu upande mmoja
Mgongo upande mmoja
Uso (hasa sehemu ya jicho)
Shingo au bega
Muhimu: Mkanda wa jeshi haupitii mstari wa kati wa mwili. Hushambulia upande mmoja tu.
Sababu za Mkanda wa Jeshi
Chanzo kikuu cha ugonjwa huu ni virusi vya Varicella-Zoster, ambavyo huwa vamelala mwilini baada ya mtu kuugua tetekuwanga. Sababu zinazochochea virusi hivi kuamka ni pamoja na:
Kushuka kwa kinga ya mwili – kutokana na:
Umri mkubwa (zaidi ya miaka 50)
Magonjwa sugu kama kisukari, VVU, kansa
Msongo wa mawazo sugu
Matumizi ya dawa zinazopunguza kinga (steroids, chemotherapy)
Matatizo ya mfumo wa neva
Msongo wa akili na uchovu mwingi
Tiba ya Mkanda wa Jeshi
1. Dawa za hospitali
Antiviral: Acyclovir, Valacyclovir au Famciclovir – huzuia virusi kusambaa zaidi na kupunguza muda wa ugonjwa.
Dawa za maumivu: Paracetamol, ibuprofen, au dawa maalum kwa maumivu ya mishipa.
Dawa za kupaka: Zinasaidia kukausha malengelenge na kupunguza maambukizi.
2. Tiba Asili na Njia za Nyumbani
Kupumzika vya kutosha
Maji ya uvuguvugu yenye chumvi – kusafisha eneo lililoathirika.
Kupaka aloe vera – hupunguza maumivu na kuharakisha kupona.
Tumia nguo laini zisizokandamiza ngozi.
3. Kinga
Chanjo ya shingles – hupendekezwa kwa watu wenye miaka 50 na kuendelea ili kuzuia mkanda wa jeshi au kupunguza ukali wake.
Muda wa Kupona
Mkanda wa jeshi hupona ndani ya wiki 2 hadi 4. Hata hivyo, baadhi ya watu huendelea kuhisi maumivu kwa miezi au miaka (hii huitwa Postherpetic Neuralgia). Ni muhimu kutibu mapema ili kuepuka tatizo hili.
Je, Mkanda wa Jeshi Unaambukiza?
Ndiyo, lakini si kwa kila mtu. Mtu aliyeathirika anaweza kuambukiza virusi vya Varicella-Zoster kwa mtu ambaye hajawahi kuugua tetekuwanga au kupokea chanjo yake. Mtu huyo ataambukizwa tetekuwanga, si mkanda wa jeshi.
Njia za kuambukiza:
Kugusana na malengelenge
Kugusana na maji kutoka kwenye vipele
Njia za Kujikinga na Mkanda wa Jeshi
Pata chanjo ya shingles
Jiepushe na msongo wa mawazo
Lala vizuri na pumzika vya kutosha
Kula lishe bora kuimarisha kinga
Epuka mgusano na watu wenye vipele vya mkanda wa jeshi, hasa kwa watoto au wajawazito
Maswali Yaulizwayo Mara kwa Mara (FAQs)
Je, mkanda wa jeshi unaambukiza?
Ndiyo, hasa kwa watu ambao hawajawahi kuugua tetekuwanga au kupata chanjo yake.
Ni kwa muda gani mkanda wa jeshi hukaa mwilini?
Huchukua wiki 2 hadi 4 kupona, lakini maumivu yanaweza kuendelea kwa muda mrefu zaidi.
Mtu anaweza kuugua mkanda wa jeshi mara ngapi?
Ingawa ni nadra, baadhi ya watu wanaweza kuupata zaidi ya mara moja.
Je, kuna tiba ya kudumu ya mkanda wa jeshi?
Hakuna tiba ya kuondoa kabisa virusi, lakini dawa hupunguza madhara na kuruhusu ngozi kupona haraka.
Chanjo ya mkanda wa jeshi hupatikana wapi?
Hospitali na vituo vya afya vikubwa vinaweza kuwa na chanjo, hasa kwa watu wenye umri wa miaka 50+.
Naweza kutumia dawa za asili peke yake?
Zinaweza kusaidia kupunguza maumivu na kuwasha, lakini dawa za hospitali ni muhimu zaidi.
Je, mkanda wa jeshi unaweza kuua?
Si rahisi kuua, lakini unaweza kusababisha matatizo makubwa kama upofu au ulemavu wa mishipa kama hautatibiwa.
Je, mkanda wa jeshi huwapata watoto?
Ni nadra, lakini unaweza kuwapata watoto waliowahi kupata tetekuwanga.
Mtu mwenye VVU yuko hatarini zaidi?
Ndiyo. Watu wenye kinga dhaifu wako katika hatari kubwa zaidi ya kupata mkanda wa jeshi.
Naweza kufanya kazi kama nina mkanda wa jeshi?
Ni bora kupumzika na kujiepusha na watu hadi malengelenge yakauke kabisa ili kuepuka maambukizi.

