Ini ni mojawapo ya viungo muhimu sana katika mwili wa binadamu. Linahusika na kazi nyingi muhimu kama kutakasa damu, kuhifadhi virutubisho, kusaidia mmeng’enyo wa chakula, na kutengeneza protini zinazosaidia kuganda kwa damu. Kwa sababu hiyo, uharibifu au ugonjwa wowote wa ini unaweza kuathiri kwa kiwango kikubwa afya ya mtu.
Ugonjwa wa ini unaweza kuwa wa ghafla (acute) au wa muda mrefu (chronic), na mara nyingi huanza kwa dalili zisizo kali ambazo ni rahisi kupuuzwa. Ni muhimu sana kugundua dalili za mwanzo mapema ili kupata matibabu sahihi kabla ya ini kuharibika zaidi.
Dalili za Mwanzo za Ugonjwa wa Ini
Zifuatazo ni dalili ambazo mara nyingi huonekana mwanzoni mwa ugonjwa wa ini, lakini watu wengi huzipuuzia au kuchanganya na magonjwa mengine:
1. Uchovu Usio wa Kawaida
Hali ya kuchoka kupita kiasi hata bila kufanya kazi ngumu ni moja ya dalili kuu za mwanzo za ini linaloanza kudhoofika.
2. Kupungua kwa Hamu ya Kula
Mgonjwa huanza kupoteza hamu ya kula bila sababu ya moja kwa moja.
3. Kichefuchefu na Kutapika
Virusi au sumu zinaposhambulia ini huathiri mmeng’enyo wa chakula, na hivyo kusababisha kichefuchefu au kutapika.
4. Maumivu ya Tumbo Upande wa Kulia Juu
Ini likianza kuvimba au kuumia, husababisha maumivu au hisia ya kujaa upande wa juu wa kulia wa tumbo.
5. Kuvimba Tumbo au Miguu
Ini likishindwa kufanya kazi vizuri, hupelekea maji kujikusanya tumboni (ascites) au kwenye miguu (edema).
6. Mkojo wa Rangi ya Giza
Mabadiliko haya ya rangi ya mkojo ni kiashiria kuwa ini linaanza kushindwa kuchuja taka mwilini.
7. Kinyesi Kuwa Chepesi au Rangi ya Udongo
Hii ni dalili ya kwamba bile (majimaji yanayotengenezwa na ini kusaidia kumeng’enya mafuta) haifiki kwenye utumbo.
8. Macho au Ngozi Kuwa ya Njano (Jaundice)
Dalili hii huanza kuonekana polepole na huonyesha kuwa ini limeanza kushindwa kusafisha bilirubin (taka ya damu).
9. Maumivu ya Misuli na Viungo
Hali ya uchovu wa mwili mzima, maumivu ya viungo au misuli huambatana na uharibifu wa ini wa awali.
10. Kuwashwa Mwili Mzima
Ini likizidiwa na sumu, hupelekea kuwashwa kwa ngozi hasa usiku.
Kwa Nini Dalili Hizi Zinaweza Kupuuziwa?
Dalili nyingi za mwanzo za ugonjwa wa ini zinafanana na magonjwa mengine ya kawaida kama mafua, malaria au maambukizi ya kawaida ya tumbo. Hii ndiyo sababu watu wengi huchukua muda mrefu kabla ya kufanyiwa vipimo vya ini. Hata hivyo, usipochukua hatua mapema, ini linaweza kuharibika kabisa bila kurudi katika hali ya kawaida.
Mambo Yanayoweza Kusababisha Ugonjwa wa Ini
Virusi: Kama Hepatitis A, B, C
Unywaji wa pombe kupita kiasi
Matumizi ya dawa kupita kiasi au zisizo sahihi
Magonjwa ya autoimmune
Mafuta mengi kwenye ini (fatty liver)
Saratani ya ini
Vipimo vya Awali vya Kugundua Tatizo la Ini
Liver Function Tests (LFTs)
Ultrasound ya tumbo
Vipimo vya virusi vya hepatitis
CT scan au MRI ya ini