Magonjwa ya zinaa (STIs – Sexually Transmitted Infections) ni magonjwa yanayoambukizwa kupitia ngono isiyo salama. Ingawa mara nyingi huonekana kuathiri zaidi wanawake, wanaume pia wako kwenye hatari kubwa ya kupata na kueneza magonjwa haya. Tatizo kubwa ni kwamba magonjwa haya yanaweza kuwa kimya (yasiyoonyesha dalili), au kuonyesha dalili zisizo wazi.
1. Maumivu au Kuungua Wakati wa Kukojoa
Dalili hii ni ya kawaida kwa magonjwa kama:
Gonorrhea
Chlamydia
Urethritis
Kama mwanaume anapata maumivu au kuchomachoma wakati wa kukojoa, ni ishara ya uambukizi kwenye njia ya mkojo.
2. Kutokwa na Majimaji Yasiyo ya Kawaida kutoka Uume
Hii ni dalili ya kawaida kwa magonjwa ya:
Gonorrhea
Chlamydia
Trichomoniasis
Majimaji haya yanaweza kuwa meupe, ya kijani au ya njano, yenye harufu mbaya. Huwa yanatoka bila msisimko wa ngono.
3. Kuvimba kwa Mapumbu au Uume
Uvimbe usio wa kawaida kwenye korodani au uume unaweza kuwa dalili ya:
Epididymitis (uvimbe wa mrija wa mbegu)
Chlamydia
Gonorrhea
Maumivu ya korodani pia huambatana na joto au wekundu katika eneo hilo.
4. Vidonda au Michubuko Sehemu za Siri
Vidonda au malengelenge kwenye uume, korodani, sehemu ya haja kubwa au mdomoni vinaweza kuashiria:
Herpes genitalis
Syphilis
Chancroid
Vidonda vya syphilis huwa haviumi mwanzoni, lakini vinaambukiza sana.
5. Kuwashwa au Harufu Mbaya Sehemu za Siri
Kuwashwa sana kwenye uume au sehemu ya haja kubwa huashiria:
Fangasi
Trichomoniasis
Bacterial infections
Wakati mwingine huambatana na harufu kali ya shombo au mkorogo.
6. Maumivu Wakati wa Kujamiiana au Kufika Kileleni
Maumivu haya yanaweza kuashiria kuvimba kwa tezi, mishipa au maambukizi kwenye njia ya uzazi. Hii ni dalili ya kawaida kwa:
Prostatitis
Gonorrhea
Chlamydia
7. Kuvimba kwa Tezi za Shingoni au Nchini ya Masikio
Tezi hizi huvimba ikiwa mwili unapambana na maambukizi kama:
Syphilis
HIV
Ni dalili ya kinga ya mwili kuwa kazini kujaribu kupambana na maambukizi.
8. Uchovu Mkubwa Usioeleweka
Kwa baadhi ya magonjwa kama HIV, uchovu wa mwili wote bila sababu ya moja kwa moja huwa dalili ya awali.
9. Homa, Kichefuchefu au Maumivu ya Kichwa
Hii hutokea hasa kwa magonjwa kama:
Hepatitis B na C
Syphilis
HIV
Dalili hizi huanza mwanzoni na zinaweza kupuuzwa kama mafua ya kawaida.
10. Kutokwa na Damu Kidogo Wakati wa Kukojoa au Kujamiiana
Ni dalili isiyo ya kawaida lakini ya kutisha. Inaweza kuashiria:
Urethritis kali
Vidonda vya ndani ya njia ya mkojo
Kansa ya uume au tezi dume (kama si ya zinaa)
MASWALI YAULIZWAYO MARA KWA MARA (FAQs)
Je, wanaume wote huonyesha dalili za magonjwa ya zinaa?
Hapana. Wengi hawaonyeshi dalili yoyote hadi pale ugonjwa unapokuwa mkubwa au kuleta madhara.
Magonjwa ya zinaa yanaweza kuathiri uzazi wa mwanaume?
Ndiyo. Magonjwa kama chlamydia na gonorrhea yanaweza kusababisha ugumba kwa kuathiri uzalishaji wa shahawa au kuziba mirija ya uzazi.
Ni muda gani dalili huanza kuonekana baada ya kuambukizwa?
Inategemea na aina ya ugonjwa. Baadhi huanza ndani ya siku 2-5 (gonorrhea), wengine ndani ya wiki kadhaa (syphilis, HIV).
Je, magonjwa haya yanaweza kupona kabisa?
Ndiyo, mengi yao yanatibika kabisa kwa dawa. Lakini baadhi kama herpes na HIV hayaponi, bali hudhibitiwa.
Naweza kumuambukiza mwenza wangu hata kama sina dalili?
Ndiyo. Magonjwa mengi huambukiza hata kama huna dalili yoyote.